Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Rais wa Korea Kusini Park Geun-hye amewasili nchini Uganda, ikiwa ni ziara yake ya pili katika taifa la Afrika yenye shabaha ya kupanua wigo wa kibiashara na fursa za uwekezaji. Rais Park Geun-hye alikaribishwa jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebe na waziri mwenye kuhusika na masuala ya nje wa Uganda Sam Kutesa. Hii ni ziara ya kwanza kufanywa kwa rais wa Korea Kusini tangu mataifa hayo yaanzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1963. Park anatokea Ethiopia, ambapo aliuhutubia Umoja wa Afrika na vilevile Jumatatu hii ataelekea Kenya. Uganda inahitaji sana wawekezaji wa kigeni kwa lengo la kustawisha uchumi wake wa kiviwanda. Rais Kaguta Yoweri Museveni amekuwa akiyalenga mataifa ya bara la Asia kama China na Korea Kusini kwa uwekezaji katika sekta kadhaa kama vile ya madini na usindikaji wa mazao yatokanayo na kilimo.
Mwisho wa habari/ 291